Imebadilishwa mara ya mwisho Mei 20, 2021
Shirika la Afya Duniani (WHO) liliutangaza mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya COVID-19 (maarufu pia kama virusi vipya vya corona) kuwa ulioenea kote duniani, yaani pandemic mnamo Machi 11, 2020. Hali duniani inaendelea kubadilika, na mataifa yanaongeza au kulegeza vikwazo vya usafiri na/au hatua nyingine za kujikinga huku aina mpya za virusi vya corona zikiendelea kutambuliwa na mipango ya kuwapa watu chanjo ya COVID-19 kushika kasi, kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari.
Wanahabari kote duniani wanatekeleza jukumu muhimu katika kuufahamisha umma kuhusu virusi hivi na juhudi za serikali za kukabiliana na virusi hivyo. Hii ni licha ya majaribio ya serikali katika mataifa kadha kudhibiti uhuru wa kuripoti na kupata habari, kama ilivyonakiliwa na CPJ. Wanahabari wanakabiliwa na shinikizo kubwa na mara kwa mara wanakuwa hatarini ya kuambukizwa kupitia kusafiri, kufanya mahojiano, na pia katika maeneo ambayo wanafanyia kazi, kwa mujibu wa mahojiano ya CPJ na wanahabari. Wanahabari wamezuiwa kutoa habari, kuzuiliwa, kushambuliwa kimwili na mtandaoni, na kupoteza mapato kutokana na COVID-19, kama ilivyoangaziwa katika ripoti za hivi karibuni za CPJ.
Ili kufahamu ushauri wa karibuni zaidi na masharti yanayowekwa, wanahabari wanaoripoti kuhusu mlipuko huu wanafaa kufuatilia taarifa kutoka kwa WHO na za mamlaka za afya nchini mwao.
Kwa maelezo ya karibuni zaidi kuhusu mlipuko huu, Kituo cha Habari Kuhusu Coronavirus cha Chuo Kikuu cha John Hopkins ni chanzo salama na cha kutegemewa.
Kujiweka salama ukiwa kazini kuripoti
Marufuku dhidi ya usafiri wa kimataifa na/au hatua nyingine za kuzuia kusambaa kwa maambukizi zinabadilika mara kwa mara. Hii ina maana kuwa kazi za kuripoti, zinaweza kubadilika kukiwa na ilani ya muda mfupi au bila notisi yoyote.
Wahudumu wa vyombo vya habari ambao wamepewa chanjo wanafaa kutambua kuwa bado wanaweza kusambaza virusi hivyo, kwa mujibu wa Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Marekani (CDC), na kwamba chanjo mbalimbali hutoa viwango tofauti vya kinga dhidi ya aina tofauti za virusi hivyo, kwa mujibu wa Yale Medicine. Hatua za kujiweka salama dhidi ya COVID-19, kama vile kukaa umbali na kuvalia barakoa, kwa hivyo zinafaa kuendelea kuzingatiwa.
Wanahabari wanaopanga kuripoti kuhusu janga la COVID-19 wanafaa kuzingatia ushauri ufuatao kuhusu usalama wao:
Kabla ya kwenda kuripoti
- Iwapo inapatikana, ni vyema kupata chanjo ya COVID-19 mapema kabla ya kwenda kuripoti ikiwa ni salama kwako, hasa iwapo utakwenda kuripoti katika au utasafiri eneo lenye hatari kubwa ya maambukizi.
- Kwa kutegemea kiwango cha hatari ya kuambukizwa katika eneo lako na unakoenda, mahojiano yanafaa kufanywa kwa njia ya simu au kupitia mtandao badala ya kukutana na anayehojiwa ana kwa ana ili kupunguza hatari ya kusambaza na/au kuambukizwa.
- Kwa mujibu wa CDC, wazee na watu wenye matatizo mengine ya kiafya kama vile kisukari na tatizo la unene wamo kwenye hatari kubwa. Iwapo umo kwenye makundi hayo, na kwa kutegemea kiwango cha maambukizi, unafaa kujiepusha kushiriki katika kazi ya kwenda kuripoti kuhusu virusi hivi ambayo itakukutanisha na umma. Wafanyakazi wajawazito wanafaa pia kutohusishwa.
- Wakati wa kuwachagua watu wa kuripoti kuhusu janga la COVID-19, wasimamizi wanafaa kutilia maanani uwezekano wa visa vya mashambulio ya ubaguzi wa rangi dhidi ya watu wa baadhi ya asili, kama ilivyoangaziwa na The New York Times.
- Vikwazo vya usafiri duniani na masharti yaliyowekwa ya kuwazuia watu kutoka nje na kutangamana vinaweza kubadilika kukiwa na ilani ya muda mfupi au bila hata notisi. Jadili ni mipango gani ambayo wasimamizi wako wanayo ya kukusaidia iwapo utaugua ukiwa kazini kuripoti, na uzingatie pia uwezekano wa kujitenga na/au kujipata kwenye eneo ambalo watu wamezuiwa kutoka/kuwekwa kwenye karantini kwa kipindi kirefu
Afya ya kiakili
- Wanahabari wote, hata wale wenye uzoefu sana, wanaweza kutatizika kiakili wanaporipoti kuhusu mlipuko wa COVID-19, kwa mujibu wa Taasisi ya Reuters katika Chuo Kikuu cha Oxford. Wasimamizi wanafaa kuwafuatilia wanahabari wao mara kwa mara kujua hali yao, na kutoa ushauri na usaidizi iwapo na wakati unapohitajika
- Fikiria athari za kiakili zinazoweza kutokana na kuripoti kutoka eneo lililoathiriwa na COVID-19, hasa iwapo unaripoti kutoka kituo cha afya au kituo cha kuwatenga watu, au eneo ambalo watu wamezuiwa kutoka nje. Maelezo muhimu kwa wanahabari wanaofanya kazi katika mazingira hatari na ya kutia kiwewe yanaweza kupatikana kupitia kituo cha DART Center cha Uanahabari na Kiwewe. Tembelea ukurasa wa Dharura wa CPJ kwa rasilimali zaidi kutoka vyanzo vya nje kuhusu kujiweka salama, zikiwemo ushauri wa kujiweka salama kiakili kama mwanahabari anayeripoti kuhusu COVID-19.
Kujikinga dhidi ya Maambukizi & Kuwaambukiza wengine
Mataifa mengi yanaendelea kutekeleza ushauri wa watu kutokaribiana, ingawa umbali unaohitajika unaweza kuwa tofauti kwa kutegemea taifa husika. Iwapo unatokea eneo lenye hatari kubwa ya kuambukizwa, kama maeneo yafuatayo hapa chini, uliza awali kuhusu hatua za usafi na usalama ambazo zinatekelezwa humo. Ukiwa na shaka zozote, usizuru:
- Kituo chochote cha afya
- Kituo au makao ya kuwatunza wazee
- Nyumbani kwa mtu yeyote anayeugua, mjamzito, au mtu aliye na matatizo ya kiafya,
- Eneo lolote la kazi mbapo hatari ya kuambukizwa inaaminika kuwa juu (kwa mfano kiwanda cha nyama)
- Mochari au chumba cha kuhifadhia maiti, tanuu ya kuchomea maiti, au panapofanyiwa ibada ya wafu
- Karantini, eneo walimotengwa watu, au eneo ambalo watu hawaruhusiwi kuingia au kutoka
- Maeneo yanayoishi watu wengi mijini (kwa mfano mtaa wa mabanda)
- Kambi ya wakimbizi au kituo cha kuwazuilia watu/gerezani palipo na visa vingi vya COVID-19
- Jela au kituo cha kuwazuilia watu ambapo kumeripotiwa visa vya COVID-19
Ushauri wa kawaida wa kujikinga na maambukizi
- Kaa umbali uliopendekezwa kati yako na wengine, ambao ni tofauti kwa kutegemea ushauri wa kiafya kutoka mamlaka hadi nyingine. Unafaa kuwa makini zaidi hasa ukiwa karibu na watu walio na dalili za ugonjwa wa kupumua, kwa mfano kukohoa na kupiga chafya na/au unapowahoji wazee, wale walio na matatizo mengine ya kiafya, mtu yeyote aliyemkaribia mgonjwa anayeonyesha dalili, wahudumu wa afya wanaowahudumia wagonjwa wa COVID-19, na watu wanaofanya kazi kwenye eneo lolote la hatari kubwa.
- Jaribu kuwahoji watu katika maeneo yaliyo wazi. Iwapo utahitajika kufanya mahojiano ndani ya nyumba, chagua pahala ambapo pana mtiririko mzuri wa hewa (mfano karibu na madirisha yaliyo wazi) na ujiepushe na vyumba vidogo au maeneo yasiyo na nafasi kubwa
- Jiepushe kumsalimia mtu yeyote kwa mikono, pamoja na kukumbatiana na kupigana busu
- Jaribu kusimama ukiwa umegeuka kidogo badala ya kumwangalia unayemhoji ana kwa ana, na ukumbuke kila wakati kukaa umbali wa uliopendekezwa.
- Osha mikono yako vyema mara kwa mara kwa maji moto na sabuni, kwa muda wa angalau sekunde 20. Hakikisha mikono yako imekaushwa kwa njia nzuri. Mwongozo muhimu kuhusu jinsi ya kuosha na kukausha mikono yako vyema upapatikana katika tovuti ya WHO
- Iwapo hauna maji moto na sabuni, tumia vitakasa mikono au vitambaa vyenye kemikali ya kuua bakteria, lakini hakikisha kwamba baadaye unaosha mikono kwa maji moto na sabuni ukipata fursa hiyo (CDC inapendekeza watu watumie vitakasa mikono vyenye kilevi cha angalau 60% ethanol au 70% isopropanol. Usitumie matumizi ya vitakasa mkono kama mbadala wa kuosha mikono mara kwa mara
- Kumbuka kufunika mdomo wako na pua unapokohoa au kupiga chafya. Unafaa kukohoa au kupiga chafya ukitumia karatasi ya shashi yaani tissue na uhakikishe unaitupa pahala salama mara moja, na kisha ukumbuke kuosha mikono vyema baadaye
- Jiepushe kujigusa uso, pua, mdomo, masikio na kadhalika
- Jiepushe kunywa/kula kwa kutumia vikombe, sahani, uma au vijiko ambavyo huenda vimetumiwa au kuwa karibu na watu wengine
- Nywele zote zinafaa kufunikwa vyema. Iwapo una nywele ndefu, zinafaa kufungwa na kufunikwa vyema.
- Vua vito vyote na mapambo pamoja na saa kabla ya kwenda kazini kuripoti, ukikumbuka kwamba virusi hivi vinaweza kusalia vikiwa hai kwenye vitu vya aina nyingi kwa muda tofauti tofauti
- Iwapo huwa unavalia miwani, isafishe kwa makini mara kwa mara kwa kutumia maji moto na sabuni
- Usivalie lensi zinazoambatanishwa na mboni za macho ukiwa kazini kuripoti, ikiwezekana, kutokana na uwezekano wako wa kuyagusa macho yako na linaweza kuongeza uwezekano wako kuambukizwa
- Fikiria ni nguo gani utavalia, kwa kuzingatia kwamba baadhi ya vitambaa vitaweza kupanguswa kwa wepesi kuliko vingine. Mavazi yote yanafaa kuvuliwa kwa umakinifu na kuoshwa kwa maji moto na kwa kutumia dawa kali au sabuni ya kusafishia baada ya kutoka kuripoti
- Ikiwezekana, jaribu kujiepusha kutumia pesa taslimu ukiwa kazini kuripoti, na uhakikishe unasafisha au kutakasa kadi zako za benki, kipochi, na/au mkoba wako mara kwa mara. Jiepushe kuweka mikono yako kwenye mifuko yako kadiri inavyowezekana.
- Fikiria kuhusu njia yako ya kusafiri kwenda na kurudi kutoka eneo unaloenda kuripoti. Ikiwezekana, jiepushe na usafiri wa umma nyakati za watu wengi kusafiri na pia hakikisha unatakasa mikono yako kwa kutumia vitakasa mikono unaposhuka.
- Iwapo unasafiri kwa kutumia gari lako au gari la kampuni, fahamu kwamba mtu yeyote aliyeambukizwa ndani ya gari hilo anaweza kuwaambukiza wengine ndani ya gari hilo. Hakikisha mkiwa safarini madirisha ya gari yako wazi kuwezesha mtiririko mzuri wa hewa ndani ya gari, na ikiwezekana mvalie vitambaa vya usoni au barakoa mkiwa ndani ya gari
- Pumzika mara kwa mara na uzingatie viwango vya nguvu/sukari mwilini mwako, ukikumbuka kwamba watu waliochoka wana uwezekano mkubwa sana wa kufanya makosa katika kudumisha usafi. Pia, zingatia kwamba watu wanaweza kuhitajika kusafiri mwendo mrefu kabla na baada ya kazi
Vifaa vya Kukinga Mwili (PPE)
Kwa kutegemea kazi yako ya kuripoti ni ya aina gani, waandishi na wahudumu wengine vya vyombo vya habari wanaweza kuhitajika kuvalia vifaakinga au PPE za kimatibabu za aina mbalimbali. Hizi zinaweza kuwa kwa mfano glavu za kutupwa baada ya kutumiwa, barakoa au mask, aproni za kujikinga/ovaroli/ vazi maalum la kukinga mwili dhidi ya maambukizi linaloufunika mwili wote, na vifunikia viatu na kadhalika.
Kuvalia na kuvua vifaa kinga vyovyote vile kwa njia salama ni jambo linalohitaji mtu kufuata ushauri wa kiusalama kwa umakinifu. Tafadhali bofya hapa kusoma ushauri kutoka kwa CDC. Unafaa kuwa makini zaidi unapovua vifaakinga, kwani wakati huo ndio hatari ya kuambukiza ilipo juu zaidi. Iwapo una shaka, tafuta ushauri wa wataalamu na upokee mafunzo kabla ya kwenda kazi yoyote ile kuripoti
Fahamu kuwa katika baadhi ya mataifa kunaweza kuwa na uhaba wa vifaakinga vya kimatibabu vilivyo bora na hivyo basi ni vigumu kupata vifaa hivyo, kwa hivyo kuvitumia kunaweza kuchangia uhaba zaidi.
- Hakikisha PPE yoyote unayoivaa inakutoshea vyema. Vifaa kinga visivyokutoshea vyema vinaweza kuraruka au kupasuka na/au kukuzuia kutembea au kufanya shughuli nyingine (iwapo vitabana sana), na pia vinaweza kukwamilia vyenye vitu kama vile kipete cha kufunga au kufungua mlango na pia kuraruka (iwapo ni kubwa zaidi haijakutoshea vyema au inapwaya)
- Kila wakati hakikisha unatumia vifaakinga vya kimatibabu vya kampuni zinazotambulika, na uzingatie sana viwango vya chini zaidi vya kiusalama vinavyohitajika. Fahamu kuwa zipo zilizo na kasoro au zilizo ghushi. Unaweza kupata baadhi ya nembo zinazoongoza na zinazotambulika sana hapa.
- Tumia glavu za kujikinga iwapo unafanya kazi katika au unatembelea kituo kilichoambukizwa kwa mfano kituo cha kuwatibu wagonjwa. Fahamu kuwa glavu za nitrile zinatoa kinga ya juu zaidi kuliko za latex. Kuvalia glavu mbili kila mkono kunaongeza kinga
- Iwapo unaripoti kutoka katika eneo la hatari kubwa kama vile kituo cha kuwatibu wagonjwa, kuna uwezekano mkubwa kwamba utahitaji PPE za kimatibabu kama vile vazi maalum la kukinga mwili dhidi ya maambukizi linaloufunika mwili wote na barakoa za ziada
- Iwapo unatumia bwelasuti au vazi linaloufunika mwili wote, hakikisha umekwenda haja msalani kabla ya kuivalia PPE hiyo
- Kwa kutegemea kazi yako ya kuripoti, unaweza ukahitaji viatu vya kuvaliwa kwa muda au buti zisizoingiza maji za kuvaliwa juu ya viatu vya kawaida, na vyote ni lazima vipanguswe/kuoshwa baada yako kuondoka eneo lililoathiriwa na virusi. Iwapo unatumia buti zisizoingiza maji, zinafaa kutupwa kwa njia salama kabla ya kuondoka eneo hilo
- Inashauriwa kwamba PPE zote za kimatibabu zivaliwe chini ya uangalizi wa mtaalamu aliyepokea mafunzo, kwa kuzingatia kwamba huu unaweza kuwa wakati wa kukumbana na virusi. Video hii ya kuvalia na kuvua vifaa kinga kutoka kwa CDC inaweza kufaa, ingawa haifai kutumiwa kama mbadala wa kupewa mafunzo/kuwa na mwangalizi
- Usitumie PPE za kutumiwa mara moja zaidi ya mara moja kwa mfano glavu, mavazi ya kukinga mwili, aproni, au vifunikia viatu. Vifaa vyote ambavyo vinahitajika kutumiwa tena ni lazima viafishwe na kutakaswa vyema. Hakikisha PPE zote zilizovaliwa zimetupwa kwa njia ifaayo KABLA ya kuondoka eneo lililoathiriwa
Barakoa au mask
Kutumia mask au barakoa ipasavyo ni muhimu sana kwa wahudumu wa vyombo vya habari wanaoripoti kutoka maeneo yenye watu, kwenye maeneo yaliyofungana, na/au katika maeneo yenye hatari zaidi ya kuambukizwa. Unafaa kufahamu kwamba kiwango cha matone yenye virusi hewani katika maeneo yenye watu wengi au yasiyo na mtiririko mzuri wa hewa kinaweza kuwa cha juu kuliko kawaida, na hivyo hilo linaweza kuongeza hatari ya kuambukizwa.
Fahamu kuwa zisipotumiwa vyema, kuna wasiwasi kwamba barakoa zinaweza kuwa chanzo cha maambukizi. Utafiti wa Lancet unaonyesha kulikuwa na masalio ya virusi kwenye barakoa ya kimatibabu kufikia siku saba baada ya kuwa kwenye eneo lenye virusi. Kwa kuzingatia utafiti huu, kuvua au kutumia tena barakoa, au kuugusa uso wako unapokuwa umevalia mask kunaweza kukuweka hatarini ya kuambukizwa.
Iwapo utavalia barakoa, unafaa kufuata ushauri ufuatao:
- Iwapo unaripoti ukiwa katika eneo lisilo na mtiririko mzuri wa hewa, au ukiwa umewakaribia wengine au ukiwa eneo lenye hatari ya juu ya kuambukizwa, unashauriwa kuvalia barakoa aina ya N95 (au FFP2/FFP3) badala ya barakoa ya kawaida ya wakati wa upasuaji.
- Hakikisha kwamba barakoa hiyo inatoshea vyema kutoka kwenye juu ya pua hadi kwenye kidevu, na kupunguza mianya.
- Hakikisha kwamba umenyoa ndevu na masharafa ili kuhakikisha barakoa inaunata na kukaa vyema kwenye uso wako.
- Ni muhimu sana kufuata ushauri wa kiusalama kikamilifu unapoitumia barakoa. Jiepushe kuigusa barakoa upande wa nje, na uivue tu kwa kuvuta kamba zake. Kadhalika, epuka kujaribu kuibadilisha badilisha au kujaribu kuiweka sawa mask yako baada ya kuivalia ila tu iwapo itabidi. Osha mikono yako papo hapo iwapo utaigusa mask yako.
- Kutumia barakoa zaidi ya mara moja ni hatari kubwa. Hakikisha unaitupa mask yako mara moja baada ya kuitumia kwa kuiweka ndani ya mfuko unaofungika.
- Osha mikono kwa sabuni na maji moto, au kwa kutumia kemikali ya kutakasa mikono iliyo na kilevi (zaidi ya 60% kwa ethanol au 70% kwa isopropanol) baada ya kuvua barakoa
- Badilisha mask kwa nyingine mpya iliyokauka baada ya ile unayotumia kulowa au kuwa na majimaji
- Kumbuka kwamba matumizi ya barakoa ni sehemu moja tu ya kujikinga. Jiepushe kugusa uso wako, pua na macho na uhakikishe unaosha mikono yako mara kwa mara kwa maji moto na sabuni.
- Fahamu kwamba barakoa zinaweza kuadimika na/au bei yake kupanda pakubwa, kwa kutegemea eneo
Usalama wa Vifaa
Kuna hatari ya kusambazwa kwa COVID-19 kupitia vifaa na mitambo iliyoambukizwa. Vifaa vyote vinafaa kuoshwa vyema na kutakaswa wakati wote:
- Tumia maikrofoni zinazoweza kunasa sauti ukiwa mbali, maarufu kama ‘fishpole’ iwapo inawezekana. Maikrofoni ndogo za kuvaliwa na anayehojiwa zinafaa kutumiwa tu katika mazingira yaliyodhibitiwa pekee, na watu wafuate ushauri wa usalama wa kiafya kikamilifu.
- Vifuniko vya maikrofoni vinafaa kutakaswa na kuoshwa vyema kwa sabuni na maji moto baada ya kurejea kutoka kazi yoyote ya kuripoti. Tafuta ushauri/mafunzo kuhusu jinsi ya kuvitoa vifuniko kwa njia salama kutoka kwa maikrofoni kuzuia kusambazwa zaidi kwa virusi Jaribu kutotumia vifuniko ‘vya manyoya’ ikiwezekana kwani inaweza kuwa vigumu kuviosha na kuvitakasa
- Tumia vidude vya kusikilizia vya gharama ya chini ikiwezekana na vitupwe baada ya kutumiwa, hasa kwa wageni. Pangusa na kutakasa vifaa vyote vya kusikilizia kabla na baada ya kutumiwa
- Tumia lensi zinazoweza kunasa picha au video kutoka mbali ili kukusaidia kukaa umbali ufaao ukiwa kazini
- Ikiwezekana, tumia vifaa vinavyopeperusha mawasiliano au data kupitia hewani badala ya zinazotumia nyaya
- Fikiria jinsi ya kuhifadhi vifaa vyako ukiwa kazini kuripoti. Usiache kitu chochote kikae kiholela na hakikisha umeweka kila kifaa kwenye sanduku au mkoba wake na kufungia vyema (kwa mfano, tumia mikoba migumu ya kusafiria kwenye ndege ambayo huwa rahisi kupangusa na kuiweka ikiwa safi)
- Ikiwezekana, tumia vifungashio vya plastiki au kitu kingine cha kufunika au kukinga vifaa vyako unapovitumia. Hii itapunguza sehemu za vifaa vyako ambazo zinaweza kuambukizwa, na itakuwa rahisi kusafisha na kutakasa baadaye
- Beba betri za ziada zilizojaa chaji na uepuke kuweka chaji ukiwa eneo uliloenda kuripoti, kwani vifaa vya kuchajia vitakuwa ni vitu vya ziada vinavyoweza kuambukizwa
- Kila wakati, takasa vifaa vyako kwa kemikali za kuua bakteria haraka kama vile Meliseptol, na baadaye uhakikishe pia unavisafisha vifaa vyote zikiwemo simu za mkononi, tablet, vihifadhia data yaani hard drives, kamera, vitambulisho na kamba za kufungia vitambulisho
- Hakikisha vifaa vyote vimetakaswa tena unapovirejesha afisini mwenu, na kuhakikisha kwamba wanaovihifadhi wanafahamishwa mapema na kwamba wamefunzwa jinsi ya kuvitakasa vifaa hivyo. Hakikisha kwamba vifaa haviwekwi tu kiholela afisini bila kuhakikisha vimekabidhiwa mtu anayefaa kuvisafisha na kuvitakasa
- Iwapo mtatumia gari wakati wa kuripoti, hakikisha kwamba limesafishwa vyema kwa undani na watu waliofunzwa vyema baada ya kurejea kutoka kazi ya kuripoti, ikiwezekana na mtu aliyepewa mafunzo vyema. Uangalizi zaidi unafaa kuwa kwenye sehemu zinazoguswa sana na watu kama vile vipete vya kufungulia milango, kifaa cha kubadilishia gia, handibreki, usukani, vioo vya kuangalia nyuma, misamilo yaani head rests, mikanda ya usalama, dashibodi, na vitufe au vidude vya kupandishia na kushushia vioo vya gari
Kuvisafisha Vifaa vya Kielektroniki
Hapa chini tumeorodhesha baadhi ya mambo unayoshauriwa kuzingatia kwa kawaida wakati wa kuvisafisha vifaa vyako vya kielektroniki. Hakikisha kila wakati kwamba umesoma mwongozo wa mtengenezaji wa kifaa kabla ya kujaribu njia yoyote ya kukisafisha.
- Kila wakati toa/chomoa kifaa kutoka kwenye nguvu za umeme, vifaa vingine, na nyaya
- Usiweke vitu viowevu au majimaji karibu na kifaa chako, na usitumie vipulizaji vya erosoli, kemikali za kupausha au kuondoa rangi na kufanya kitu kuwa cheupe, na vitu vinavyochubua au kukwaruza – kwani sana sana hivi vyote vitaharibu kifaa chako
- Usipulizie kitu chochote moja kwa moja kuelekea kwenye kifaa chako
- Tumia kitambaa kisichokwaruza, laini na kisichokuwa na nyuzi za pamba
- Kifanye kitambaa chako kiwe na unyevu kidogo, lakini KISILOWE. Mwagia au kupaka sabuni kwenye kitambaa na uisugue kwa mkono wako kwenye kitambaa
- Pangusa kifaa chako vyema mara kadha kwa kutumia kitambaa hicho
- Usikubali unyevu wowote ufikie matundu au mashimo yoyote (kwa mfano matundu ya kuwekea chaji, vitundu vya kuingizia vifaa vya kusikilizia, na kibodi)
- Kausha kifaa chako kwa kukipangusa kwa kutumia kitambaa safi kilichokauka na kilicho
- Baadhi ya watengenezaji wa vifaa hupendekeza matumizi ya vitaa vya kupangusia vyenye kilevi aina ya isopropyl kwa kiwango cha 70% kusafisha maeneo ya vifaa yasiyoingiza unyevu
- Iwapo unatakasa vifaa vyako, ni vyema kutafuta ushauri wa mtengenezaji wa vifaa hivyo kwanza, kwani vitakasa vinaweza kuharibu kifaa chako.
Unaweza kupata ushauri zaidi na wa kina kupitia taarifa hii.
Usalama wa kidijitali
- Fahamu kwamba wanahabari wanakabiliwa na viwango vya juu vya uadui mtandaoni kutokana na wanavyoripoti kuhusu mlipuko wa COVID-19. Wanaweza kushambuliwa na makundi ya watu wanaopinga chanjo au wanaopinga uvaaji wa barakoa. Soma ushauri wa CPJ kuhusu njia za kujikinga dhidi ya mashambulio mtandaoni
- Serikali na kampuni za teknolojia wanatumia upelelezi wa kuwafuatilia na kuwachunguza watu kama njia ya kufuatilia kusambaa kwa COVID-19. Hii ni pamoja na NSO Group, ambayo imeunda Pegasus, ambayo ni programu ya kijasusi ambayo imetumiwa kuwaandama wanahabari, kwa mujibu wa Citizen Lab. Makundi ya kutetea haki za kiraia yameeleza wasiwasi wao kuhusu jinsi teknolojia hizi zitakavyotumika kuwafuatilia watu baada ya mzozo huu wa kiafya kumalizika. Shirika la Transparency International limekuwa likifuatilia matukio haya kwenye tovuti yao
- Wahalifu wanaendelea kutumia mgogoro huu wa kiafya kuwaandamana wanahabari na mashirika yenye njama na mifumo ya utapeli kuhusiana na utoaji wa chanjo yameongezeka, kwa mujibu wa ripoti. Simama na kufikiria kabla ya kubofya kwenye kiunganisho au link mtandaoni au kupakua nyaraka zinazodaiwa kuwa na maelezo kuhusu COVID-19 au chanjo kwani mashambulio ya barua pepe za kutumiwa kama chambo yaani phishing emails yanaweza kusababisha programu hasidi au zenye madhara kuwekwa kwenye vifaa vyako vya kielektroniki, kwa mujibu wa Electronic Frontier Foundation
- Kuwa makini sana unapobofya kwenye viunganisho au link zozote kuhusu COVID-19 kwenye mitandao ya kijamii au app za kuwasiliana kwa kutumia ujumbe, baadhi ambazo huenda zikakuelekeza kwenye tovuti zinazoweza kuambukiza kifaa chako programu hasidi au zenye madhara
- Kuwa makini kuhusu taarifa za uzushi ambazo zinaweza kuwa zinaenezwa na vyombo vya serikali, kama ilivyoripotiwa na The Guardian, pamoja na taarifa za uzushi za kawaida, jambo ambalo WHO imetahadharisha sana kuhusu na BBC imeangazia. Mwongozo wa kutambua habari hizi za uzushi unapatikana katika mtandao wa WHO
- Soma kuhusu kuwasiliana na kuandaa mikutano kupitia mtandao na masuala ya faragha ili kufahamu huduma hizi zinafanya nini na data yako, wanaweza kupata data gani kutoka kwako, na ni salama kiasi gani. Fahamu kuwa huku watu wanaofanyia kazi manyumbani mwao ikiongezeka, huduma hizi zimelengwa na wadukuzi
- Tahadhari kuhusu hatari zinazotokana na kuripoti kuhusu na/au kutoka mataifa yenye uongozi wa kiimla, ambayo kuna uwezekano yatakuwa yanafuatilia kwa karibu ripoti kuhusu mlipuko wa COVID-19. Baadhi ya serikali zinaweza kujaribu kuficha ukweli kuhusu kuenea kwa mlipuko na/au kuzuia vyombo vya habari kuripoti ukweli, kama ilivyoangaziwa na CPJ
Uhalifu & usalama wako ukiwa kazini kuripoti
- Iwapo unaweza kusafiri kwenda kuripoti nje ya nchi yako (soma hapa chini), tafiti kuhusu hali ya karibuni zaidi ya kiusalama unakoenda. Zingatia kwamba kumekuwepo na visa vya ghafla vya ghasia na maandamano maeneo mbalimbali duniani tangu mwanzo wa janga hili. Baadhi wa waandishi wameripoti kushambuliwa kwa maneno na wengine hata kuandamwa na wahalifu, kwa hivyo usipuuze usalama wako.
- Kuwa mwangalifu zaidi iwapo unaripoti kutoka maeneo ya mashambani. Watu wanaweza kuwashuku “watu kutoka nje” kwa hofu kuwa huenda wakawa wamebeba virusi
- Fahamu kuwa kuna uwezekano wa polisi kutumia nguvu kupita kiasi wakitekeleza maagizo ya watu kutotoka nje kutokana na COVID-19, na uzingatie hatari ya kupigwa na kutumiwa kwa mabomu ya kutoa machozi
- Wanahabari katika mataifa yenye serikali za kiimla wanafaa kufahamu na kuzingatia hatari ya kuzuiliwa, kukamatwa na/au kufurushwa kutoka nchi husika wakiripoti kuhusu mlipuko wa COVID-19, kama ilivyoangaziwa na CPJ
Kwenda kuripoti nje ya nchi
Kutokana na marufuku na vikwazo vya usafiri vilivyotolewa na mataifa mengi duniani, inaendelea kuwa vigumu kusafiri nje ya nchi. Hata hivyo, iwapo inawezekana kwenda kuripoti nje ya nchi yako, unafaa kuzingatia yafuatayo:
- Chunguza iwapo kuna/au kunapangwa marufuku za usafiri eneo unalopanga kusafiri, ukifahamu kwamba hali inaweza kubadilika kwa notisi fupi.
- Fahamu kuwa hatua za kuwazuia watu na/au amri ya kutoka nje zote zinaweza kuwa tofauti kutoka sehemu moja ya nchi hadi nyingine. Fahamu kuwa hatua za kuwazuia watu zinaweza kutekelezwa kukiwa na notisi ya muda mfupi au hata bila notisi, kwa hivyo kila wakati fuatilia vyanzo vya habari vya eneo hilo kufahamu yanayojiri.
- Hatua za kuwaweka watu wanaorejea nchi fulani karantini zinaweza kuanza kutekelezwa au kubadilishwa kukiwa na ilani ya muda mfupi au bila ilani yoyote kwa kutegemea taifa unaloelekea na eneo ulilolitembelea
- Vitambue vituo vyote vya matibabu vilivyo eneo unakofanya kazi. Ukizingatia kuwa wahudumu wa afya wanaweza kugoma au kufanya maandamano wakiwa wametoa notisi ya muda mfupi au bila notisi hata kidogo
- Huenda kukawa na uhaba wa PPE na/au hata ziwe hazipatikani hata kidogo, na/au ubora wake uwe wa kutiliwa shaka. Hakikisha kwamba kila wakati unafanya utafiti mapema kabla ya kusafiri, na kujibebea za ziada ikiwa itahitajika.
- Ikiwezekana, jaribu kupata chanjo ya COVID kabla ya kwenda kuripoti na uhakikishe umetimiza masharti yote ya chanjo na kinga za magonjwa yanayohitajika katika taifa hilo kwa wakati.
- Angalia vyema bima yako ya usafiri, ukifahamu kwamba huenda ikawa vigumu kupata bima ya kusafiri maeneo yaliyo na COVID-19. Fahamu kuwa mataifa mengi yametoa ushauri na tahadhari za viwango tofauti dhidi ya kusafiri kuingia mataifa hayo.
- Mara kwa mara angalia yanayojiri kuhusu hafla yoyote unayopanga kuhudhuria, kwa kuzingatia kwamba mataifa mengi yamepiga marufuku mikusanyiko ya watu kuanzia kiasi fulani.
- Mataifa mengi yameendelea kufunga mipaka yake. Mipaka inayoweza ikafunguliwa inaweza pia kufungwa tena bila tahadhari, jambo ambalo unafaa kulizingatia wakati wa kuandaa mpango wako wa kuchukua hatua wakati wa dharura.
- Usisafiri iwapo unaugua. Viwanja vingi vya kimataifa na kikanda, pamoja na vituo vingi vya usafiri, vimetekeleza masharti makali ya watu kupimwa afya yao.
- Fahamu kuwa COVID-19 imesababishia mashirika ya ndege hasara kubwa kifedha, kwa mujibu wa taarifa za habari, kwa hivyo fikiria uwezekano wa kununua tiketi za ndege ambazo unaweza kurejeshewa nauli yote ukikosa kusafiri.
- Angalia hali ya karibuni zaidi kuhusu viza unakoenda, ukitambua kwamba mataifa mengi yamesitisha utoaji wa viza
- Chunguza iwapo taifa unakoenda linahitaji cheti cha kimatibabu cha kuthibitisha kwamba hauna COVID-19.
- Kuwa na ratiba inayoweza kubadilishwa kwa urahisi na utenge muda wa ziada wa kupitia viwanja vya ndege maeneo mbalimbali, kwa kuzingatia vipimo vya ziada vya afya na vituo vya kupima watu joto. Vilevile katika baadhi ya vituo vya treni, bandari/gati, na vituo vya usafiri wa mabasi ya masafa mrefu
Baada ya kuripoti
- Fuatilia hali yako ya afya mara kwa mara kubaini iwapo una dalili
- Huenda ukalazimika kujitenga baada ya kurejea kutoka kuripoti kutoka eneo lenye hatari kubwa. Tafadhali chunguza ushauri husika wa serikali
- Fuatilia taarifa na habari za karibuni zaidi kuhusu COVID-19, pamoja na utaratibu wowote wa karantini au kujitenga unaotekelezwa unakotoka na unakoenda
- Kwa kutegemea kiwango cha maambukizi katika taifa ulilomo, unafaa kutafakari uwezekano wako kuweka shajara au kitabu kidogo chenye majina/nambari za simu za watu ambao unatangamana nao kwa siku 14 baada yako kurejea. Hii itasaidia katika kuwatafuta iwapo utaanza kuonyesha dalili za kuambukizwa
–Iwapo una dalili za kuugua
- Iwapo utaanza kuonyesha au utapata dalili za COVID-19, hata ziwe ndogo, wafahamishe wasimamizi wako. Shirikiana nao kuchukua hatua zifaazo kusafiri kutoka hatua ya mwisho ya safari yako ya kuripoti hadi kwako nyumbani. Usichukue tu teksi ya kawaida
- Fuata ushauri wa WHO, na CDC, au mamlaka za afya nchini humo kujikinga na kuwakinga wengine
- Usiondoke kwako nyumbani kwa angalau siku 7 kuanzia siku dalili za kuugua zilipoanza kujidhihirisha (muda ambao utahitajika kutotoka kwako nyumbani ni tofauti kutoka nchi hadi nyingine, na hubadilika pia). Kufanya hivyo kutasaidia kutowaambukiza wengine
- Jiandae mapema na uwaombe wengine usaidizi iwapo utahitaji. Mwombe mwajiri wako, na jamaa na marafiki wakusaidie kupata bidhaa unazozihitaji, na waziache nje ya mlango wako
- Weka umbali salama ulioshauriwa kati yako na watu wengine nyumbani mwako ikiwezekana, na iwapo itawezekana lala peke yako
Kifurushi cha Usalama cha CPJ kinawapa wanahabari na mashirika ya habari maelezo mengi ya msingi kuhusu usalama wa wanahabari kikiangazia mwili, akili na dijitali, na pia kinaangazia jinsi ya kuripoti kuhusu fujo za raia na uchaguzi.
[Angalizo la mhariri: Ushauri huu ulichapishwa mara ya kwanza mnamo Februari 10, 2020, na unafanyiwa mabadiliko mara kwa mara. Tarehe ya kuchapishwa inayoonyeshwa pale juu inaonyesha tarehe ya karibuni zaidi ya mabadiliko.]