Na Muthoki Mumo/Mwakilishi wa CPJ Afrika kusini mwa Sahara
Mwaka wa 2017, Simon Mkina alikuwa ndiye mchapishaji na pia mhariri mkuu wa gazeti la habari za uchunguzi Tanzania la Mawio wakati serikali ilipotangaza kuwa imesimamisha uchapishaji wa gazeti hilo kwa “kuhatarisha usalama wa taifa” kwa kuchapisha ripoti ya kutuhumiwa kwa marais wawili wa zamani kuhusika katika sakata la madini. Mkina alilazimika kujiachisha kazi, pamoja na wafanyakazi wengine 57, na akawa mwandishi wa habari wa kujitegemea.
Marufuku hiyo ilifaa kudumu kwa miaka miwili pekee, lakini iliendelea kwa muda zaidi baada ya mamlaka kukosa kuiondoa hata baada ya mahakama kuamua kuwa ilikuwa “kinyume cha sheria” na “isiyo na msingi.” Lakini, mwezi Februari, serikali ilibadilisha msimamo. Nape Nnauye, waziri wa habari wa Tanzania aliyeteuliwa hivi majuzi, alitangaza kwamba amerejesha leseni ya gazeti la Mawio, pamoja na leseni za magazeti ya MwanaHALISI, Mseto, na Tanzania Daima, ambayo ni machache tu kati ya magazeti yaliyokuwa yamepigwa marufuku ama kusimamishwa kuchapisha habari mtandaoni au gazetini chini ya uongozi wa aliyekuwa Rais John Pombe Magufuli.
“Kama nimekuja nasema nia yetu njema, tuanze kwa kufungua ukurasa mpya,” Nnauye alisema Februari 10 katika mkutano na wahariri wa vyombo vya habari Dar es Salaam, jiji kuu la kiuchumi Tanzania. Nnauye alisema alikuwa anatekeleza maagizo ya rais mpya, Samia Suluhu Hassan, aliyemrithi Magufuli baada ya kifo chake mwaka mmoja uliopita. Serikali hiyo mpya ambayo pia imeyafungia magazeti, inalenga kufanya kazi kwa pamoja na waandishi wa habari kufanyia mageuzi sheria za vyombo vya habari Tanzania, alisema Nnauye. Alipoombwa na CPJ kueleza zaidi kuhusu mageuzi hayo, msemaji wa serikali Gerson Msigwa alisema yangetangazwa baadaye.
CPJ ilizungumza na Mkina kuhusu mipango yake ya kufufua gazeti lake, na maana ya kuondolewa kwa marufuku hiyo kwa uhuru wa waandishi wa habari Tanzania. Mahojiano hayo yamehaririwa kuyafupisha na kuyafanya yaeleweke vyema zaidi. Mahojiano yalifanywa kwa Kiingereza lakini tumeyatafsiri.
Ulipokeaje habari kwamba leseni ya Mawio ilikuwa imerejeshwa?
Simon Mkina: Nilipokea habari hizo kutoka kwenye mitandao ya kijamii. Nilipata hisia za nafuu kubwa kutokana na uwezekano wa kuweza kurudi katika uchapishaji na kuifanya kazi niipendayo zaidi. Ni kana kwamba uhuru umerejeshwa baada ya kucheleweshwa kwa miaka mitano.
Nini ilikuwa matokeo ya marufuku ya miaka mingi ya Mawio?
Athari kubwa zaidi ilikuwa kwa wananchi. Haki yao ya uhuru wa kupata habari ilikiukwa. [Mwaka 2017] watu wengi walifika katika afisi zetu [kueleza wasiwasi wao kutokana na kufungwa kwa gazeti]. Baadhi ya taasisi, yakiwemo mashirika ya wanasheria na watetezi wa haki za kibinadamu, ziliandika barua kupinga kupigwa marufuku kwa gazeti hilo. Katika mitandao ya kijamii kulikuwa na simulizi nyingi kutoka kwa wasomaji wetu waliokuwa wanailaumu serikali kwa uamuzi huo. Umma nao, ndani na nje ya nchi, ulitetea kurejeshwa kwa gazeti hilo.
Gazeti hilo lilipopigwa marufuku, wafanyakazi waliendelea kufanya kazi kama waandishi?
Tulilazimika kufunga afisi zetu kwa sababu hatukuwa na biashara nyingine tuliyokuwa tunajihusisha nayo isipokuwa uandishi. Waandishi, wahariri, wasanifishaji kurasa, na wafanyakazi wengine kama vile madereva, wote waliachwa bila kazi. Katika afisi yetu kuu Dar es Salaam, tulikuwa [wafanyakazi] 27. Na tulikuwa na waandishi katika mikoa yote Tanzania bara, pamoja na visiwani Zanzibar. Kwa hivyo, kwa jumla watu 57 waliachwa bila kazi kutokana na kufungwa kwa gazeti hilo. Athari zake ni zaidi ya kwa watu hao 57, kwani wana familia [zilizowategemea]. Ni waandishi wachache sana waliofanikiwa kuendelea na uanahabari, ilikuwa vigumu kupata kazi nyingine.
Uliendelea kufanya kazi kama mwandishi, na kazi zako zikachapishwa kwa mfano katika gazeti la kila wiki la The Mail & Guardian la Afrika Kusini. Ilikuwaje kwako kubadilika kutoka kuwa mhariri na kuwa mwandishi wa kujitegemea?
Haikuwa rahisi. Lakini ukweli ni kuwa: lazima uishi. Lazima uwalee watoto wako. Hakuna biashara nyingine ninayoifahamu vyema kuliko uanahabari. Lakini haikuwa tu kuishi, ninaipenda taaluma hii.
Tunaweza kutarajia kuliona gazeti la Mawio likiuzwa tena karibuni au bado kuna vikwazo vilivyosalia?
Itachukua muda kiasi kwa Mawio kuanza kuchapishwa tena, kwani kunahitajika mtaji kiasi kikubwa. Tunahitaji kuanza upya. Tunahitaji bajeti ya kupiga chapa, ambayo ni zaidi ya shilingi za Tanzania milioni 100 [US$43,300] kwa miezi kadha, hata kabla ya gazeti kuweza kujisimamisha kifedha na kujitengenezea mapato. Tunahitaji mitambo na vifaa pia na pia kuajiri wafanyakazi. Kwa hivyo kuna kazi kubwa iliyosalia. Tayari tumeanza kufanya baadhi ya mambo hayo – kutafuta wafanyakazi na afisi mpya.
Nafasi ya Mawio katika sekta ya habari Tanzania itakuwa gani litakapoanza kuchapishwa tena?
Tukifanikiwa kurejea, Mawio itaendelea kufuatilia habari ambazo huwa haziripotiwi kwingine katika vyombo vikuu vya habari. Tutaangazia uandishi wa upekuzi, uandishi wa uchunguzi. Siwezi nikasema ni mada gani tutaangazia kwa wakati huu – lakini katika kila habari huwa kuna fursa ya uchunguzi iwapo unataka kuangazia habari kwa undani, iwe ni kuhusu masuala ya kijamii, kifedha au kiutawala.
Unaweza kuelezea vipi mazingira ya uhuru wa uandishi wa habari tangu Samia alipokuwa rais mwaka mmoja uliopita?
Rais Samia amepiga hatua kubwa kutoka kwenye kile ninachoweza kueleza kuwa enzi ya giza katika uhuru wa vyombo vya habari Tanzania. Alianza kwa kuonyesha ishara njema kuhusu uhuru wa vyombo vya habari na kuna mtiririko wazi wa habari kwa wananchi. Lakini bado kuna kazi kubwa inayohitajika kufanywa.
Nchi yetu ina sheria tata za vyombo vya habari ambazo katika uhalisia zitakuwa kikwazo katika mazingira yetu ya kazi. Lakini bado nina matumaini kwamba Rais Samia atazifanyia kazi na kurekebisha. Ni muhimu sasa kwamba sheria husika, ikiwa ni pamoja na Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari [sheria ya mwaka 2016 iliyobainishwa kuwa kikwazo kwa uhuru wa uandishi wa habari na Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ)] zifanyiwe marekebisho.
Muthoki Mumo ni mwakilishi wa CPJ Afrika kusini mwa Sahara. Hufanyia kazi Nairobi, Kenya, na ana shahada ya uzamili katika uandishi na utandawazi kutoka Chuo Kikuu cha Hamburg.