Rais wa Tanzania ambaye ndiye mgombea urais wa chama tawala Chama Cha Mapinduzi (CCM) John Magufuli (kati) akiwasili kutoa hotuba wakati wa uzinduzi rasmi wa kampeni za chama hicho kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Oktoba jijini Dodoma, Tanzania, mnamo Agosti 29, 2020. Mamlaka ya mawasiliano Tanzania imeviandama vyombo vya habari kwa faini na kuvifungia kabla ya uchaguzi. (AFP/Ericky Boniphace)

Uchaguzi ukikaribia mamlaka ya mawasiliano Tanzania inatumiwa kama fimbo dhidi ya vyombo vya habari

Na Muthoki Mumo/Mwakilishi wa CPJ Africa kusini mwa Sahara

Mnamo Agosti 27, siku ya pili ya kipindi rasmi cha kampeni Tanzania bara kuelekea uchaguzi wa Oktoba 28, mamlaka ziliamrisha vituo vya Clouds TV na Clouds FM kuahirisha matangazo yao ya kawaida na badala yake kuomba radhi mfululizo hadi saa sita usiku na baada ya hapo kusitisha matangazo kabisa kwa wiki moja.  

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ilitoa adhabu hiyo isiyo ya kawaida, kwa msingi kuwa vituo hivyo viwili vilikuwa vimekiuka sheria kwa kupeperusha matokeo ya uteuzi wa wagombea wa ubunge bila kuthibitisha taarifa hizo na Tume ya Uchaguzi Tanzania.

Adhabu za aina hii zimeanza kuwa kawaida Tanzania. Mwaka 2020, TCRA imeamrisha takriban televisheni moja ya mtandaoni, tovuti moja ya habari, na takriban vituo vingine vinne kusitisha matangazo kwa muda, na kupiga faini takriban vyombo vingine 10 vya habari, kwa mujibu wa utathmini wa taarifa za umma za TCRA uliofanywa na CPJ. Mamlaka hiyo ilitaja kupeperushwa kwa maudhui ya kutisha na maudhui kuhusu ngono kama sababu iliyoifanya kuadhibu baadhi ya vituo; vingine viliadhibiwa kwa kudaiwa kuripoti kwa njia ya kupotosha au ya kupendelea upande mmoja kuhusu mada kama vile siasa na janga la COVID-19

Msimamo mkali wa mamlaka hiyo – ambao ndilo tukio la karibuni zaidi katika kudorora kwa miaka mingi kwa uhuru wa wanahabari Tanzania ilivyonakiliwa na CPJ – kunaathiri uwezo wa wanahabari kuripoti kuhusu uchaguzi mkuu ujao kwa njia huru, kwa mujibu wa wanahabari zaidi ya kumi nchini Tanzania waliozungumza na CPJ Septemba na Oktoba.

“Kuna mazingira ya wasiwasi – woga mwingi uliowaingia wanahabari. Hatua ya kujidhibiti wenyewe inatokea. Watu wengi huamua ni heri kutotenda baadhi ya mambo badala ya kuyatenda nawe uwe hatarini ya kuadhibiwa na TCRA au wizara [ya habari],” alisema Jenerali Ulimwengu, mwandishi wa makala katika gazeti la kila wiki la TheEastAfrican ambaye pia ni mbunge wa zamani nchini Tanzania.

Ulimwengu, aliyewasiliana na CPJ kupitia WhatsApp Septemba na Oktoba, alisema anafikiri vyombo vya habari vinaogopa na kujizuia kukosoa Chama Cha Mapinduzi (CCM), chama tawala Tanzania.

Rais John Magufuli anawania kuchaguliwa tena dhidi ya wagombea wengine 14, kwa mujibu wa ripoti. Uchaguzi unapokaribia, mamlaka nchini Tanzania zimezidisha juhudi zao za kukabiliana na mashirika ya kiraia na upinzani, na kuibua wasiwasi miongoni mwa waangalizi wa siasa na mashirika ya haki kwamba mazingira nchini humo “hayatafanikisha uchaguzi huru na wa haki” kama ambavyo Ringisai Chikohomero, mtafiti katika shirika lisilo la kutengeneza faida la Institute for Security Studies, anavyoeleza.  

Waandishi wa habari waliozungumza na CPJ Desemba 2015 walikuwa na matumaini kwamba rais mteule Magufuli angebadilisha sheria za uhalifu wa kimitandao na sheria za takwimu zilizokuwa zinatishia uhuru wa wanahabari na pia kusitisha sheria tata ya vyombo vya habari iliyokuwa inapendekezwa. Badala yake, katika miaka mitano iliyopita CPJ imenakilikudorora sana kwa uhuru wa wanahabari kupitia mashtaka ya kulipiza kisasi kufungiwa kwa vyombo vya habari kiholela, na sheria zinazominya uhuru

Mwezi Julai, Tanzania ilifanyia marekebisho kanuni zake za maudhui ya mtandao za 2018, na kusisitiza hitaji la watoaji habari mtandaoni wakiwemo wanablogu, kulipa ada za juu za usajili kwa TCRA na kuongeza vikwazo kwenye vitengo vingi vya maudhui, ikiwemo maandamano ya siasa na majanga, kwa mujibu wa kanuni hizo ambazo CPJ imezitathmini. Kanuni hizo zilizofanyiwa marekebisho pia zinaipa TCRA, inayojieleza kama “Taasisi ya Serikali iliyo na uhuru kiasi” iliyoanzishwa mwaka 2003 kusimamia vyombo vya habari vya kielektroniki na kusimamia masafa ya mawasiliano, nguvu za kusimamia utekelezaji.

“TCRA imekuwa zaidi ya mamlaka ya kusimamia na kuchukua majukumu yanayoegemea sana upande wa kuzuia [usambazaji wa habari]” Maria Sarungi-Tsehai, mkurugenzi wa kituo huru cha Kwanza Online TV, aliambia CPJ kupitia WhatsApp mwezi Septemba.

Khalifa Said, mwanahabari huru aliyezungumza na CPJ mwezi Septemba, alikumbuka akimhoji mpigavideo wa kufanya kazi naye kwenye mradi fulani ambaye alikuwa na wasiwasi sana kiasi kwamba aliomba kuwekwe kifungu kwenye mkataba wake wa kazi cha kumuondolea lawama iwapo mamlaka zitachukua hatua.

Maafisa katika TCRA hawakujibu barua pepe za CPJ za kuomba tamko lao kuhusu hayo Septemba na Oktoba. CPJ pia iliwasiliana na waziri wa habari wa Tanzania, aliye na mamlaka ya kumteua mkurugenzi mkuu wa TCRA pamoja na wanachama wa bodi. Kupitia simu, waziri, Harrison Mwakyembe, alikataa kutoa tamko lolote, akisema ana shughuli nyingi kuhusiana na uchaguzi. Aliwaelekeza CPJ kwa msemaji wa serikali, Hassan Abbasi, lakini naye hakujibu ujumbe mfupi wala simu ilipopigwa na CPJ.

Aprili TCRA ililifungia Mwananchi, gazeti linalochapisha habari kwa Kiswahili, kutochapisha habari zozote mtandaoni kwa miezi sita kwa kosa la kuchapisha video ya zamani ya Magufuli akiwa kwenye soko la samaki lenye shughuli nyingi. Wakati huo, watu wenye ufahamu kuhusu suala hilo waliambia CPJ kwamba video hiyo ilikuwa inafasirika kwamba ilimuonyesha rais kuwa alikuwa akifanya jambo lisilo la busara wakati wa janga la COVID-19. Mwezi Julai, mamlaka hiyo iliiadhibu Kwanza Online TV na marufuku ya miezi 11 kwa kusambaza tahadhari ya usafiri ya ubalozi wa Marekani kuhusu COVID-19, kama ilivyonakiliwa na CPJ. Mwananchi walirejelea kuwepo mtandaoni Oktoba 16, kwa mujibu wa taarifa kwenye tovuti yao na kwenye TheCitizen, gazeti linalomilikiwa na kampuni moja na gazeti hilo la Mwananchi.

Chambi Chachage, mchambuzi wa siasa za Tanzania na mtafiti katika Chuo Kikuu cha Princeton, alisema ingawa baadhi ya kanuni zinafaa, alitiwa wasiwasi na utekelezaji wa kanuni hizo kwa njia inayobadilika na kwa njia ya kiholela.

“Nani huamua kama utafungiwa kwa wiki moja? Au kufungiwa mwaka mmoja?” alisema Gachage, aliyepo Marekani, kwenye simu ya video na CPJ.

Kati ya Januari na Aprili, Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) ulinakili kushtakiwa kwa wanahabari na wanablogu wasiopungua saba, kwa kudaiwa kukosa kusajili tovuti na akaunti za YouTube na TCRA, kwa mujibu wa taarifa za umma za Mtandao huo. Mtandao huo, ambao huleta pamoja makundi wenyeji ya kutetea haki nchini humo, ulisema ulinakili jumla ya watu wasiopungua 13 walioshtakiwa kipindi hicho; wawili walipatikana na hatia na kuamua kulipa faini ya chini zaidi ya shilingi milioni tano za Tanzania (US$2,150) badala ya kwenda jela miezi 12.  

Agosti na Septemba, CPJ ilizungumza na watu watatu waliokuwa wameshtakiwa chini ya sheria hii waliosema gharama ya usajili ni ya juu mno na kwamba wanaishi na wasiwasi wa uwezekano wa kuadhibiwa. “Ni nafuu kwangu kwenda jela kwa mwaka mmoja badala ya kulipa faini hii,” alisema mwanablogu Jabir Johnson, ambaye ndiye pekee kati ya watatu hao aliyekubali kutajwa na ambaye kesi yake bado inaendelea kortini.

Mamlaka hiyo pia imeviandama vyombo vya habari vya ndani kwa kutumia maudhui ya vyombo vya kutoka nje ya nchi. Agosti, TCRA ilitoa onyo kwa vituo vinne vya redio Tanzania kwa kupeperusha mahojiano ya BBC na mgombea urais wa upinzani Tundu Lissu, kwa mujibu wa taarifa ya TCRA

Kuonywa huko kulitokea baada ya mabadiliko kwenye kanuni za utangazaji, ambayo CPJ ilitathmini, mwezi Juni ambapo sasa vituo vya ndani vinahitaji leseni kutoka kwa TCRA ili kupeperusha maudhui ambayo hayatoki ndani ya vituo hivyo. Kanuni hizo pia zina sharti lisiloeleweka vyema kwamba watangazaji wanatakiwa kumshirikisha afisa wa serikali wakati wa kutekeleza shughuli zozote na watu kutoka nchi za nje, bila ya kufafanua vyema.

Maafisa wamefafanua kanuni hizo na kusema ni njia ya kufuatilia ushirikiano wa vyombo mbalimbali na kampuni za nje na kuhakikisha kwamba maudhui kutoka nje yanatimiza viwango vinavyohitajika nchini humo, kwa mujibu wa ripoti kwenye vyombo vya habari na taarifa kutoka kwa TCRA.

“Tunasalia kuwa na wasiwasi sana kuhusu kanuni hizi mpya, kwani inaonekana kama lengo ni kudhibiti yale ambayo vyombo vya habari Tanzania vitaweza kupeperusha siku za usoni, na hivyo kuuweka umma katika nafasi isiyo nzuri,” mkuu wa Idhaa ya Afrika ya DW, Claus Stäcker, aliambia CPJ kupitia barua pepe ingawa alisema kwamba washirika wote wa utangazaji wa shirika hilo la Ujerumani nchini Tanzania walipokea vibali vipya bila kukawia.


Na mnamo Agosti 31, kwenye taarifa, USAGM, ambalo ni shirika la serikali ya Amerika linalosimamia idhaa ya Sauti ya Amerika (VOA) , lilisema baadhi ya washirika wake Tanzania “walisitisha mara moja upeperushaji wa vipindi vilivyoandaliwa nje ya nchi” kanuni hizo zilipofanywa wazi kwa umma. Kwenye barua pepe ya Oktoba 15, USAGM waliambia CPJ kwamba 23 kati ya vituo washirika 24 walivyokuwa navyo sasa wanapeperusha maudhui ya VOA; mmoja bado anasubiri kibali cha TCRA kumruhusu kufanya hivyo.

USAGM waliambia CPJ kwamba hawaamini kwamba kanuni hizo mpya za utangazaji zitakuwa na athari zozote kwenye jinsi VOA watatangaza kuhusu uchaguzi huo. Hata hivyo, waandishi wenyeji waliozungumza na CPJ hawakuwa na matumaini sana.

“Tunajaribu kudumisha utaalamu wetu na kuangazia kila upande kwa njia sawa, lakini hata hilo haliwezi kukukinga. Kwa sasa hivi, kama mwandishi, utataabika,” mwanahabari anayefanyia kazi Watetezi TV, inayomilikiwa na THRDC alisema. Mwandishi huyo aliomba asitambuliwe kwa kuogopa kuadhibiwa.